Rais wa Zambia awataka wananchi wote kupambana na ufisadi
2021-12-10 09:15:47| cri

Zambia imeungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ufisadi mwaka huu jana Alhamisi, ambapo rais wa nchi hiyo Hakainde Hichilema amewataka wananchi wote kupambana na ufisadi. 

Rais Hichilema amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni Haki Yako, Wajibu Wako, Sema Hapana kwa Ufisadi- ambayo inazingatia zaidi jukumu la kila mwananchi katika kuhakikisha tabia hiyo mbaya inaondolewa kwenye jamii.

Kiongozi huyo amesema kuondoa ufisadi ni muhimu ili kuharakisha maendeleo ya nchi kuelekea kupata ustawi wa kiuchumi na kuboresha maisha ya watu, akisisitiza kuwa vita dhidi ya ufisadi havipaswi kuachiliwa vyombo vya kisheria tu, bali vinatakiwa kuwa jukumu la kila mtu.

Pia ameongeza kuwa ufisadi ni tatizo la kimataifa, ambalo ni moja ya vitisho vya kutimiza malengo ya maendeleo endelevu na kikwazo katika kujenga Afrika yenye ustawi na amani.