Mtaalamu wa Nigeria: Maslahi mapana ya pamoja ni msingi wa ujenzi wa Jumuiya ya China na Afrika yenye Hatma ya Pamoja
2021-12-13 09:26:25| cri

Mtaalamu wa Nigeria: Maslahi mapana ya pamoja ni msingi wa ujenzi wa Jumuiya ya China na Afrika yenye Hatma ya Pamoja_fororder_QQ图片20211210151558

Mkurugenzi wa Utafiti katika Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Kimataifa ya Nigeria (NIIA) Profesa Efem N. Ubi amesema, mustakbali wa pamoja kamwe hauwezi kujengeka bila uwepo wa maslahi ya pamoja, hivyo maslahi mapana ya pamoja kati ya China na Afrika ndio msingi wa ujenzi wa Jumuiya yenye Hatma ya Pamoja inayotarajiwa na pande zote mbili.

Akihojiwa hivi karibuni na Shirika Kuu la Utangazaji la China (CMG), Profesa Ubi amesema, kwa China na Afrika, mustakbali wa pamoja hauwezi kuondokana na maendeleo ya pamoja, ambapo pande hizo mbili zinapaswa kuhimiza usawa, kuaminiana, kujaliana, kufundishana na kunufaishana kati yao kwenye ushirikiano wa kujenga jumuiya yenye hatma ya pamoja kati ya pande hizo mbili. Amesema, mkutano wa nane wa mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika mwezi Novemba huko Dakar, Senegal, ulitangaza Miradi Tisa ya ushirikiano, ikiwa ni mpango wa kwanza wa miaka mitatu kwenye Ajenda ya Ushirikiano kati ya China na Afrika ya Mwaka 2035. Anaona miradi hiyo inayolenga kuondoa matatizo, changamoto na vizuizi vilivyokuwepo kwa muda mrefu vinavyokwamisha maendeleo ya Afrika, ni maslahi ya pamoja kati ya China na Afrika.

Profesa Ubi amesema, njia pekee ya kujenga jumuiya yenye hatma ya pamoja kati ya China na Afrika ni kutafuta namna ya kuisaidia Afrika kujikwamua kwenye matatizo na changamoto zinazoikabili chini ya misaada na uungaji mkono wa China. Anaona kuwa, jumuiya hiyo inaweza kujengeka tu kwa ushirikiano wa dhati na utekelezaji halisi.