Jeshi la Somalia lawaua wanamgambo 5 wa al-Shabab katika eneo la kusini
2021-12-13 09:49:16| CRI

Vikosi vya Jeshi la Kitaifa la Somalia (SNA) vimewaua magaidi watano wa al-Shabab katika operesheni za usalama zilizoendeshwa katika eneo la kusini mwa nchi hiyo.   Makamanda wa SNA waliiambia Redio Mogadishu Jumapili kwamba maficho kadhaa ya al-Shabab pia yaliharibiwa katika operesheni hiyo iliyofanyika katika muda wa saa 24 zilizopita katika vijiji vya Gambarey, Dawacale na Geediyan katika eneo la Lower Shabelle.   "Jeshi pia liliwafukuza baadhi ya magaidi waliokuwa wakisababisha matatizo makubwa kwa wenyeji," ilisema redio hiyo inayomilikiwa na serikali huku makamanda wa SNA wakiapa kuendelea na mashambulizi hayo hadi pale vikosi vyao vitakapowaondoa wanamgambo hao katika eneo hilo.   Kwa mujibu wa redio hiyo inayomilikiwa na serikali, wanakijiji walikaribisha oparesheni za usalama zinazoendelea, wakisema wamefurahishwa na mafanikio ya sasa ya kijeshi ambayo yataleta amani katika eneo hilo.   SNA inayoungwa mkono na Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia iliwafukuza al-Shabab kutoka Mogadishu mwaka 2011, lakini kundi hilo la kigaidi bado lina uwezo wa kufanya mashambulizi, yakilenga mitambo ya serikali, hoteli, migahawa na maeneo ya umma. Enditem