China yatoa msaada wa chakula kwa Uganda
2021-12-15 09:41:06| cri

China imechangia chakula chenye thamani ya dola milioni 2 za kimarekani kupitia Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) kwa kusaidia watoto wa shule za eneo la Karamoja, kaskazini-mashariki mwa Uganda.

Mwakilishi wa WFP nchini Uganda Abdirahman Meygag amesema msaada huo ni muhimu sana kwa watoto kuendelea na masomo yao wakati shule zimefungwa kutokana na athari ya janga la virusi vya Corona kwani chakula hicho kitapelekwa nyumbani kwao.

Balozi wa China nchini Uganda Zhang Lizhong alisema kwenye sherehe ya makabidhiano kuwa China inaiunga mkono kithabiti Uganda katika juhudi zake za kuhifadhi nguvu kazi kwa ajili ya siku za baadaye. Na msaada huo wa chakula ni kama ujumbe wetu kwa kila mtoto kwenye eneo la Karamoja kwamba wakiendelea na masomo watapata chakula na kupata fursa ya kutoa mchango kwa taifa lao katika siku za baadaye.

Mwezi wa Februari mwaka huu, China ilisaini makubaliano na WFP ya kuchangia chakula zaidi ya tani elfu 3 za ujazo kwa Uganda kwa ajili ya wanafunzi zaidi ya milioni 1.2 wa shule 300 huko Karamoja.