Wawekezaji wa Afrika Mashariki wahimiza kuondolewa vizuizi vya kibiashara kati ya Kenya na Uganda
2021-12-16 09:32:56| CRI

Baraza la biashara la Afrika Mashariki EABC ambalo ni shirika kuu la sekta binafsi la kikanda, limefanya mazungumzo ya pande mbili yanayolenga kuondoa vizuizi visivyo vya ushuru kati ya Kenya na Uganda, ili kustawisha biashara za kikanda.

Mkurugenzi mtendaji mkuu wa Baraza la EABC Bw. John Bosco Kalisa amezihimiza nchi hizo kuepusha mvutano wa kibiashara na hatua za kulipiza kisasi zinazotokana na kuwekeana vizuizi vya kibiashara.

Bw. Kalisa ametoa taarifa ikisema EABC inaamini kuwa kulipiza kisasi hakutakuwa utatuzi wa mwisho, na nchi hizo mbili zinatakiwa kukaa pamoja kutatua masuala yanayostahili kutatuliwa.  

Kwa mujibu wa baraza hilo Uganda imesema itazuia baadhi ya mazao ya kilimo yaliyosindikiwa na yasiyosindikwa kutoka Kenya, kufuatia Kenya kupiga marufuku baadhi ya bidhaa za kilimo kutoka Uganda.