Waandamanaji nchini Sudan wafika ikulu wakidai utawala wa kiraia
2021-12-20 09:01:47| CRI

Maelfu ya waandamanaji nchini Sudan wamefanikiwa kuvunja kizuizi cha usalama kilichowekwa na kufika ikulu ya nchi hiyo mjini Khartoum, wakidai utawala wa kiraia katika kumbukumbu ya tatu ya mapinduzi yaliyofanyika mwezi Desemba, 2018, na kumwondoa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar al-Bashir.

Shirika la Habar nchini humo limeripoti kuwa, watu hao walifanikiwa kuvuka madaraja matatu yanayounganisha miji ya Khartoum, Bahri na Omdurman, licha ya uwepo wa vikosi vingi vya usalama. Waandamanaji hao walieleza kupinga makubaliano ya kisiasa yaliyofikiwa Novemba 21 kati ya Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la Mpito wa Sudan, Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan na Waziri Mkuu wa Mpito Abdallah Hamdok.

Wakati huohuo, Kamati ya Madaktari nchini Sudan imesema, ripoti ya awali imeonyesha kuwa mtu mmoja ameuawa na wengine 80 kujeruhiwa wakati wa maandamano hayo.