Kongamano la jumuiya za washauri bingwa kati ya China na Sudan Kusini ni mfano wa kuigwa wa ushirikiano wa kitaaluma kati ya China na Afrika
2021-12-23 09:55:31| CRI

Kongamano la jumuiya za washauri bingwa kati ya China na Sudan Kusini ni mfano wa kuigwa wa ushirikiano wa kitaaluma kati ya China na Afrika

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Sudan Kusini Bw. Deng Dau Deng Malek amesema, kuna umuhimu mkubwa kwa nchi hiyo na China kuendeleza mawasiliano na ushirikiano kwenye nyanja ya kitaaluma, kwa kuwa vitatoa mapendekezo ya kisera kwa ajili ya kusukuma mbele mchakato wa amani wa Sudan Kusini na ushirikiano kati ya nchi hiyo na China. 

Akihutubia kwa njia ya video kwenye ufunguzi wa Kongamano la pili la Jumuiya za Washauri Bingwa kati ya China na Sudan Kusini lililofanyika hivi karibuni, Bw. Malek amesema, serikali ya Sudan Kusini inaunga mkono kithabiti mawasiliano na ushirikiano kati ya jumuiya za washauri bingwa na vyuo vikuu vya nchi hizo mbili. Amesema, Sudan Kusini, ikiwa nchi changa zaidi duniani, ina maliasili na raslimali nyingi kama vile mafuta, madini, kilimo, maji, uvuvi, mifugo na wanyamapori. Hivyo anatumai kuwa wasomi na wataalamu wa nchi hizo mbili watapanua njia mpya za ushirikiano ili kusukuma mbele maendeleo ya pande mbili. Pia wanapaswa kufuatilia zaidi nyanja nyingine ikiwemo kilimo, elimu, ujenzi wa uwezo, amani na usalama, biashara, uwekezaji na upunguzaji wa umaskini. Amesema, Sudan Kusini inakaribisha awamu ijayo ya kongamano hilo kufanyika mjini Juba, na kuweka mfano wa kuigwa kwa ushirikiano wa kitaaluma kati ya China na Afrika.

Bw. Malek amesema, Sudan Kusini ilianzisha uhusiano wa kibalozi na China siku ya kwanza baada ya kupata uhuru wake Julai 9 mwaka 2011. Katika miaka kumi iliyopita, nchi hizo mbili zimendelea kuimarisha hali ya kuaminiana kisiasa, ushirikiano halisi kati yao kwenye sekta mbalimbali umezaa matunda mengi, na kuonesha mustakbali mzuri katika siku zijazo. Amesema, kabla ya hapo aliongoza ujumbe wa serikali ya Sudan Kusini kuhudhuria mkutano wa nane wa mawaziri wa mambo ya nje wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC uliofanyika nchini Senegal, ambapo walijitahidi kushiriki na kufanikisha kutungwa na kusainiwa kwa nyaraka za matokeo ya mkutano huo. Amesisitiza mara nyingine tena kuwa Sudan Kusini inapenda kushirikiana na China katika kutekeleza vizuri matokeo yaliyopatikana kwenye mkutano huo, kuimarisha mawasiliano na ushirikiano kwa pande zote, na kusukuma mbele uhusiano kati ya Sudan Kusini na China uendelee kupiga hatua mbele.