Sudan yaziagiza mamlaka husika kufanyia uchunguzi madai ya ubakaji dhidi ya wanawake waandamanaji
2021-12-28 09:44:22| CRI

Baraza la Mpito la Utawala la Sudan jana lilizitaka mamlaka husika kuchunguza madai ya vitendo vya ubakaji dhidi ya waandamanaji wanawake vilivyofanyika Disemba 19 huko Khartoum.

Katika mkutano wa kawaida wa Baraza la Mpito la Utawala la Sudan ulioongozwa na mwenyekiti wake Abdel Fattah Al-Burhan, limezielekeza mamlaka husika kuchunguza kile kinachoendelea kusambaa kwenye vyombo vya habari juu ya tukio la ubakaji. Awali Disemba 21, Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa UM iliamuru kufanywa uchunguzi wa haraka, huru na wa kina juu ya madai ya unyanyasaji wa kingono ukiwemo ubakaji wa mtu mmoja na wa genge katika maandamano ya Disemba 19.

Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu huko Geneva Liz Throssell, amesema wamepokea ripoti zikidai wanawake na wasichana 13 walibakwa na mtu mmoja au na genge, na wanawake hao wameripotiwa kunyanyaswa kingono wakati wakikimbia eneo la karibu na ikulu ya rais mjini Khartoum.