Jeshi la China lasema malengo ya vitendo vyake huko Taiwan ni kulinda mamlaka ya nchi
2021-12-31 10:10:21| CRI

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya China Tan Kefei, amesema vitendo vya Jeshi la Ukombozi wa Watu wa China (PLA) vya majini na angani kwenye kisiwa cha Taiwan vina malengo wazi, na kuthibitisha tena azma ya jeshi hilo kulinda mamlaka ya taifa na ukamilifu wa eneo lake.

Akijibu kuhusu vitendo vya hivi karibuni vya ndege ya PLA ambavyo vimekuwa vikikosolewa na mamlaka za Chama cha Maendeleo ya Demokrasia cha Taiwan DPP, Bw. Tan amesema katika mwaka mmoja uliopita, PLA imefanya doria na mazoezi ya kijeshi majini na angani kwenye kisiwa hicho, akisema lengo liko wazi kabisa ambalo ni kuchukua hatua kali za kujilinda dhidi ya vitendo vibaya vya nguvu za ndani na nje ya kisiwa hicho vya kushirikiana na kuipinga kanuni ya China moja, kulinda mamlaka ya taifa na ukamilifu wa eneo, na kulinda kwa makini ustawi wa pamoja wa wenzao katika pande zote mbili za mlango bahari wa Taiwan na kudumisha amani na utulivu wa mlango bahari.