Tanzania yashirikisha sekta binafsi katika uzalishaji wa nishati ya upepo
2022-04-14 11:47:07| CRI

Shirika la Umeme Tanzania TANESCO linashirikisha sekta binafsi katika uzalishaji wa nishati ya upepo.

Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen. Byabato aliliambia Bunge mjini Dodoma kuwa baadhi ya wawekezaji wanatekeleza miradi ya nishati ya upepo mkoani Singida kwa kushirikiana na TANESCO. Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Jesca Kishoa, Byabato alisema umeme utakaozalishwa kutokana na nishati ya upepo utaongeza uzalishaji wa umeme nchini.

Mbunge huyo aliitaka serikali kueleza ni lini nishati ya upepo itaanza kuzalisha umeme katika mkoa wa Singida uliopo katikati mwa Tanzania.

Byabato alisema wawekezaji wapo katika hatua tofauti za utekelezaji wa miradi takriban mitatu ya nishati ya upepo mkoani Singida ambayo imepangwa kukamilika kati ya mwaka 2023 na 2027.

Alisema TANESCO imeanza kufanya mazungumzo na makampuni binafsi ya nishati ya upepo ili kuliuzia shirika hilo umeme.