Nigeria yarekodi vifo 31 katika mlipuko wa kipindupindu
2022-04-14 11:51:05| CRI

Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Nigeria (NCDC) kimesema kuwa hadi sasa takriban vifo 31 vimerekodiwa mwaka huu kutokana na ugonjwa wa kipindupindu nchini Nigeria.

Afisa mkuu wa mwitikio wa dharura wa NCDC Bi. Jessica Akinrogbe amesema kuwa nchi hiyo imerekodi jumla ya wagonjwa 1,359 waliothibitishwa kuwa na kipindupindu kuanzia mwezi Januari.

Kipindupindu ni ugonjwa hatari sana unaojulikana kwa kuanza ghafla kuharisha majimaji papo kwa hapo, ambao unaweza kusababisha kifo kutokana na upungufu mkubwa wa maji mwilini.

Bi. Akinrogbe amesema jumla ya majimbo 15 yameathirika na mlipuko huo, na kusisitiza kuwa NCDC tayari imetuma timu ili kupunguza kuenea. Wakati msimu wa mvua ukikaribia nchini humo, juhudi zaidi lazima zilenge kuzuia kuibuka tena.

Afisa huyo wa afya ya umma alihimiza kuongeza maandalizi na mpango wao wa kukabiliana na kipindupindu na kujenga uwezo wa kudhibiti matukio ya dharura.