Kenya yalaumu juhudi za nchi moja pekee ndio sababu ya kuibuka kwa ugonjwa wa malaria katika Afrika Mashariki
2022-04-15 09:13:24| CRI

Waziri wa Afya wa Kenya Mutahi Kagwe amesema juhudi za nchi moja pekee katika usimamizi wa malaria ndio jambo linalopaswa kutupiwa lawama katika kuibuka tena kwa maambukizi ya ugonjwa huo katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hayo amesema katika uzinduzi wa mapambano ya kudhibiti na kuzuia malaria ya kuvuka mpaka, uliofanyika katika mpaka wa Kenya na Uganda huko Busia, magharibi mwa Kenya, na kuongeza kuwa huu ni wakati muhimu kwa nchi wanachama kukumbatia juhudi za pamoja za kuvuka mipaka ili kupunguza na hatimaye kuangamiza malaria katika kanda hiyo.

Kagwe amesema juhudi za pamoja za nchi mbalimbali zinaweza kutoa fursa ya pekee katika kanda kwa kuwa ugonjwa wa malaria hautambui mipaka ya nchi, na kusisitiza mahitaji ya kuoanisha na kusawazisha utekelezaji wa mbinu mbalimbali za kudhibiti malaria kama vile kupuliza dawa ndani ya nyumba miongoni mwa nchi wanachama.