WHO: Afrika bado haijanasuka na COVID-19 licha ya kupungua kwa maambukizi
2022-04-15 09:11:08| CRI

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kuwa nchi za Afrika zinahitaji kuwa macho na kujua hatari kabla ya kulegeza hatua za kupambana na COVID-19, licha ya kupungua kwa maambukizi, na kwamba bara hilo linakabiliwa na hatari ya kuibuka tena kwa virusi pamoja na kuja kwa virusi vipya.

Kwenye taarifa iliyotolewa na ofisi WHO kanda ya Afrika imesema kwa wiki 16 zilizopita idadi ya wagonjwa kwa wiki imepungua, baada ya Aprili 10 kurikodi mambukizi 18,000 na vifo 239 katika wiki iliyopita, ikipungua kwa asilimia 29 na 37 mtawalia. Hata hivyo WHO imesema licha ya maambukizi kupungua, ni muhimu kwa nchi zote kuendelea kuwa macho na kudumisha hatua za ufuatiliaji, zikiwemo ufuatiliaji wa jeni ili kutambua haraka virusi vya COVID-19 na kuongeza upimaji na utoaji chanjo.

Sambamba na hilo Mkurugenzi wa Kituo cha Kuzuia na Kukinga Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) John Nkengasong naye amesisitiza kuwa nchi hazipaswi kuhadaika kwamba kwasababu zipo kwenye msimu wa mabadiliko katika Afrika na duniani kwa ujumla, ndio hazitashuhudia janga likirejea tena. Hivyo amesema zinapaswa kufuata hatua zote za kukinga COVID-19.