Afrika Kusini yatangaza hali ya janga la kitaifa ili kukabiliana na mafuriko
2022-04-19 08:46:31| CRI

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini jumatatu usiku alitangaza hali ya janga la kitaifa, kufuatia gharama ya mafuriko ya wiki yaliyouathiri vibaya mkoa wa KwaZulu-Natal kufikia mamilioni ya randi.

Akihutubia taifa kwa njia ya televisheni, rais Ramaphosa amesema Baraza la mawaziri lilikutana kwenye kikao maalumu jumapili usiku na kuamua kutangaza Hali ya Janga la Kitaifa. Wiki iliyopita, mkoa wa KwaZulu-Natal pia ulitangaza hali ya janga.

Kwa mujibu wa rais huyo, madhara ya janga hilo yamesambaa nje ya mkoa wa KwaZulu-Natal, na uharibifu wake kwa Bandari ya Durban umeleta athari za kina, ndio maana baraza la mawaziri limefikia uamuzi wa kutangaza Hali ya Janga la Kitaifa.

Inakadiriwa kuwa watu zaidi ya elfu 40 wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na mafuriko hayo, ambayo rais Ramaphosa ameyataja kuwa “janga la kibinadamu linalohitaji juhudi kubwa na za dharura za kutoa misaada”.