Somalia yapongeza China kwa kuunga mkono ukarabati wa hospitali
2022-04-20 09:28:13| CRI

Maofisa wa afya wa Somalia wameushukuru ubalozi wa China kwa kuunga mkono ukarabati wa jengo la upasuaji la hospitali ya Banadir huko Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.

Kwenye hafla ya kukamilika ukarabati mkurugenzi wa hospitali hiyo Bw. Fartum Sharif Mohamed amesema vyumba vitatu vya upasuaji, vitanda vinne vya upasuaji, taa za upasuaji na vifaa vingine vimewekwa katika ukarabati huo uliofanywa kwa miezi minne. Ameishukuru China iliyojenga hospitali hiyo na kufanya juhudi maradufu kuunga mkono na kuifanya hospitali hiyo kuwa ya kisasa.

Bw. Mohamed amesema kufuatia kurejeshwa kwa uendeshaji mwezi wa Februari, hospitali hiyo sasa ina uwezo wa kuwapokea wajawazito 200 kwa mwezi.

Hospitali ya Banadir ilijengwa na China katika miaka ya 70, na kupanuliwa katikati ya miaka ya 80, na imekuwa mfano wa kuigwa wa urafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika.