Katibu mkuu wa UM awataka Putin na Zelensky kukutana naye Moscow na Kiev
2022-04-21 09:22:27| CRI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres amewataka viongozi wa Russia na Ukraine kumpokea ili kujadili kuhusu hatua za kuleta amani kufuatia operesheni maalumu ya kijeshi inayofanywa na Russia nchini Ukraine.

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric ametoa taarifa ikisema, barua tofauti zimetumwa kwa ujumbe wa kudumu wa Russia na ya Ukraine katika Umoja huo, zikiwataka Vladimir Putin kumpokea Bw. Guterres huko Moscow na Volodymyr Zelensky kumpokea huko Kiev.

Kwa mujibu wa Dujarric, Bw. Guterres amesema katika wakati huo wa hatari, anataka kujadili hatua za dharura kuhusu amani huko Ukraine na siku za baadaye za mfumo wa pande nyingi kwenye msingi wa katiba ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.

Msemaji huyo ameongeza kuwa Bw. Guterres ameeleza kuwa Ukraine na Russia zote ni wanachama waanzilishi wa Umoja wa Mataifa, na siku zote zinauunga mkono umoja huo.