Somalia na Umoja wa Mataifa zaahidi kuongeza kasi ya kutoa chanjo kwa watoto
2022-04-25 08:40:25| CRI

Somalia na mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa pamoja zimewataka wadau wa kibinadamu, mashirika binafsi na wafadhili kusaidia kuongeza kasi ya kutoa chanjo kwa watoto nchini humo.

Wizara ya Afya ya nchini Somalia, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) zimesema, Somalia inakadiriwa kuwa na watoto 639,000 wenye umri wa chini ya mwaka mmoja, lakini wengi wao hawajapata chanjo zozote zinazotakiwa kwa watoto.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Somalia Angela Kearney amesema katika taarifa ya pamoja iliyotolewa kuadhimisha Wiki ya Chanjo Duniani, kuwa chanjo ni ulinzi dhidi ya magonjwa yanayozuilika na maisha yenye afya zaidi. Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wazazi na walezi kusimamia afya ya watoto wao kwa kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata chanjo inayotakiwa.