Uganda yahitaji fedha za dharura kwa ajili ya wakimbizi wanaoongezeka kwa kasi
2022-05-02 10:11:30| CRI

Mashirika ya msaada nchini Uganda yamesema zinahitajika fedha za dharura kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya maelfu ya wakimbizi wanaotoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Sudan Kusini.

Takwimu kutoka Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) imeonyesha kuwa tangu mwezi Januari mwaka huu, idadi ya wakimbizi wanaokimbilia Uganda imezidi asilimia 50 ya wakimbizi wapya 67,000 wanaotarajiwa ndani ya mwaka huu.

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa UNHCR nchini Uganda imesema tangu mwezi Januari mwaka huu, Uganda imepokea wakimbizi zaidi ya elfu 35, ambao theluthi moja kati yao walifika kutoka mkoa wa Kivu Kaskazini na Ituri nchini DRC ndani ya wiki tatu zilizopita.

Tarehe 29 mwezi Aprili, UNHCR na mashirika mengine 44 nchini humo yametoa ombi la dharura la dola milioni 47.8 za kimarekani, ili kukidhi mahitaji ya dharura ya wakimbizi elfu 60 kwa muda wa miezi mitatu.