UNICEF yakabiliwa na pengo la fedha za kukidhi mahitaji ya watu milioni 9.9 nchini Ethiopia
2022-05-03 09:46:44| CRI

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limebainisha kuwa limepokea asilimia 22 tu ya dola za Kimarekani milioni 351 linazohitajika ili kukidhi mahitaji ya watu milioni 9.9 nchini Ethiopia.

Katika ripoti ya Hali ya Kibinadamu iliyochapishwa na UNICEF, ilisema shirika hilo linahitaji fedha hizo ili kukidhi mahitaji ya watu milioni 9.9 walioathiriwa na hali ya ukame katika maeneo manne ya Ethiopia.

Fedha hizo zinazoombwa ni pamoja na zinazohitajika kusaidia watoto milioni 4.45 nchini Ethiopia.

UNICEF inalenga kutoa vifaa vya kuokoa maisha pamoja na usaidizi wa huduma za afya, lishe, elimu na usafi kwa wahitaji.

Taarifa ya UNICEF pia ilisema karibu watoto 650,000 wanaacha shule katika maeneo ya Oromia, Southern na Somali kutokana na hali ya ukame. Sambamba na hilo ilieleza kuwa hali ya ukame imelazimisha kufungwa kwa shule 2,000 kote nchini Ethiopia.