Kenya yaweka marufuku ya kutoka nje usiku katika mkoa wa kaskazini
2022-05-03 09:40:48| CRI

Serikali ya Kenya jana ilitangaza marufuku ya kutoka nje usiku na operesheni za usalama kwa muda wa mwezi mmoja katika kaunti ya Marsabit, kaskazini mwa nchi hiyo, ili kuimarisha zoezi la upokonyaji silaha kutokana na kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na usalama.

Waziri wa Usalama wa Ndani Bw. Fred Matiang'i amesema kaunti ndogo ya Komu iliyoko karibu na kaunti ya Isiolo na eneo la Sololo lililoko karibu na mpaka kati ya Kenya na Ethiopia pia itaathiriwa na marufuku hiyo. Amesema wameona kuna uhusiano kati ya kuenea kwa bunduki huko Marsabit na vurugu za Komu, ambako uchimbaji haramu unafanyika.

Marufuku hiyo inayoanza saa 12 jioni hadi saa 12 asubuhi itaendelea kwa siku 30, na muda huo unaweza kurefushwa. Wakati huohuo, zoezi la kunyang’anya silaha haramu litafanyika.