Katibu mkuu wa UM aahidi kuunga mkono mahitaji ya msaada wa kibinadamu ya Jimbo la Borno Nigeria
2022-05-05 10:40:49| CRI

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza dhamira yake ya kuunga mkono hatua za kuboresha hali ngumu ya wakimbizi wa ndani (IDPs) katika Jimbo la Borno, Nigeria.

Guterres amesema hayo huko Maiduguri, mji mkuu wa Jimbo la Borno na kitovu cha kundi la waasi Boko Haram, ambapo alifuatilia watu walioathiriwa na uasi uliodumu kwa mwongo mmoja na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuunga mkono Jimbo la Borno kushughulikia mahitaji ya kibinadamu. 

Guterres ambaye awali alitembelea Senegal na Niger kama sehemu ya “Ziara yake ya mshikamano ya Ramadhani” barani Afrika, aliwasili Nigeria Jumanne na kutembelea baadhi ya kambi za IDPs na maeneo ya mpito ya wanamgambo wa kundi la Boko Haram huko Borno.

Alisema ikiwa msaada huo utatolewa, kundi la Boko Haram litatoweka kwani uungaji mkono wa jumuiya ya kimataifa utaisaidia serikali ya Jimbo la Borno kuipa matumaini ya maendeleo na imani, ambapo wananchi wanaona kuwa mustakabali wao unaweza kuaminika.