Watumishi wa afya wa Sudan Kusini na China watangaza umuhimu wa siku ya usafi wa mikono duniani
2022-05-06 10:14:49| CRI

Watumishi wa afya wa Sudan Kusini wakishirikiana na wenzao Wachina jana walitangaza umuhimu wa usafi wa mikono ndani ya vituo vya afya kwa lengo la kuzuia na kudhibiti magonjwa ya kuambukiza. Hatua hiyo inakwenda sambamba na hatua ya Shirika la Afya Duniani kutangaza Siku ya Usafi wa Mikono Duniani.

Mario Damba, Mhudumu wa chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Mafunzo ya Juba, ameipongeza timu ya tisa ya madaktari wa China kwa kutumia siku hiyo kuhamasisha watumishi wa afya na wagonjwa juu ya umuhimu wa kuosha mikono.

Naye muuguzi wa China, Jiang Shijun ambaye ameshuhudia zoezi la kuhamasisha katika hospitali kuu ya rufaa, amesema tukio hilo linalenga kusisitiza wafanyakazi wenzake wa Sudan Kusini juu ya umuhimu wa kuboresha usafi wa mikono kwa watumishi wa afya na pia kuzuia maambukizi wanayopata hospitalini.