Tanzania yapanga kuacha kuagiza sukari na mafuta ya kupikia kabla ya mwaka 2025
2022-05-10 09:18:04| CRI

Waziri wa kilimo wa Tanzania Bw. Hussein Bashe, na waziri wa uwekezaji, viwanda na Biashara Bibi Ashatu Kijaji, wamesema serikali ya Tanzania ina mpango wa kuacha kuagiza sukari na mafuta ya kupikia kabla ya mwaka 2025.

Mawaziri hao wamesema hayo kwenye mkutano wa bunge unaoendelea mjini Dodoma. Bw. Bashe amesema hatua za muda mfupi za kupunguza uagizaji wa mafuta ya kupikia ndani ya miaka mitatu ni pamoja na kusambaza mbegu za alizeti zenye ruzuku kwa wakulima wadogo, na za muda mrefu ni pamoja na motisha wa kikodi kwa wakulima wakubwa wa michikichi.

Bibi Kijaji amesema serikali inafanya juhudi kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwenye sekta ya uzalishaji wa sukari na mafuta ya kupikia na viwanda vya usindikaji wa bidhaa hizo.

Kwa sasa matumizi ya mafuta ya kupikia nchini Tanzania ni tani laki 6.5 kwa mwaka, lakini uzalishaji ni tani laki 2.5, matumizi ya sukari ni tani laki 4.7 lakini uzalishaji ni tani laki 3.7.