Katibu mkuu wa UM alaani mashambulizi dhidi ya raia nchini DRC
2022-05-10 09:26:58| CRI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres amelaani vikali mashambulizi dhidi ya raia yaliyofanywa jumapili iliyopita na kundi lenye silaha nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC.

Msemaji wa katibu mkuu Bw. Stephane Dujarric ametoa taarifa ikisema Bw. Guterres amelaani vikali mashambulizi yaliyofanywa na kundi la Shirikisho la maendeleo la Kongo katika sehemu ya Djugu mkoani Ituri.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, raia 38 wa kawaida wakiwemo wanawake na watoto wameuawa katika kituo cha uchimbaji wa madini cha Blakete-Plitu. Raia wengi wamekimbia makazi yao na wameripotiwa kutojulikana walipo baada ya  washambuliaji hao kuteketeza kijiji cha Malika kilichoko karibu.

Jana tume ya umoja wa mataifa ya kulinda amani nchini DRC MONUSCO ilifanya operesheni ya utoaji wa matibabu kwa raia waliojeruhiwa vibaya.