Kenya yapigania kupanda misitu ili kukabiliana na msukosuko wa kiikolojia barani Afrika
2022-05-11 08:42:23| CRI

Katibu mkuu wa wizara ya mazingira na misitu ya Kenya Bw. Chris Kiptoo, amesema kuna haja kwa nchi za Afrika kusini mwa sahara kuanzisha mipango yenye nguvu ya kurudisha misitu ili kukabiliana na msukosuko wa kiikolojia.

Akiongea mjini Nairobi kwenye uzinduzi wa mradi wa FLaRAK wenye hatua za kurudisha misitu na ardhi wa Kenya, Bw. Kiptoo amesema msukosuko wa kimazingira unahitaji mbinu za kivumbuzi kama kurudisha misitu.

Amesema kurudisha misitu na ardhi ni suluhisho la asili lililothibitishwa linaloweza kusaidia kufikia malengo ya maendeleo endelevu. Pia amesema Kenya inawekeza kwenye sekta za mazingira na misitu kwa kuwa sekta hizo ni msingi wa ongezeko la uchumi, kutokana na kuunga mkono sekta za uzalishaji viwandani, nishati, afya na kilimo.

Amesema Kenya imejiwekea mpango kabambe wa uwiano wa uharibifu wa ardhi kufikia sifuri ifikapo mwaka 2030 na kurudisha karibu hekta milioni 5.1 za ardhi.