Wanaharakati watoa mwito wa kukomesha ufugaji wa Simba wakati tishio kwa wanyama hao likiongezeka
2022-05-12 08:46:28| CRI

Ufugaji wa Simba kwenye mazingira ya kufungiwa unaotokana na ongezeko la mahitaji kwenye sekta za dawa mbadala na mapambo, unatakiwa kukomeshwa ili kuwaokoa Simba kwenye mapori ya Afrika.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa mjini Nairobi na makundi la harakati ya ulinzi wa wanyama World Animal Protection na Blood Lions, imesema ukatili wanaofanyiwa Simba kwenye maeneo wanayofugwa kwa kufungiwa ni sababu ya kutaka kukomeshwa kwa ufugaji huo, na wanyama hao wanatakiwa kuishi kwa uhuru kwenye mazingira yao ya asili.

Ofisa wa kampeni kuhusu wanyamapori wa World Animal Protection Bibi Edith Kabesiime, amesema sheria zinatakiwa kutungwa ili kupiga marufuku ufugaji wa Simba kwa kuwafungia.

Ameipongeza Afrika Kusini kwa kuahidi kuacha ufugaji huo wa Simba hatua kwa hatua, na kusema kupiga marufuku kamili ya biashara ya viungo vya Simba ikiwa ni pamoja na mifupa, kutasaidia kuongeza idadi yao maporini.