UM waonya kuhusu kuongezeka kwa idadi ya watu wanaokabiliwa na ukosefu wa chakula Afrika Mashariki
2022-05-12 09:05:15| CRI

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa idadi ya watu wanaokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na maji katika eneo la Afrika Mashariki huenda itaongezeka hadi kufikia milioni 20.

Ofisi ya uratibu wa mambo ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA, imesema zaidi ya watu milioni 15 wanakabiliwa na msukosuko wa chakula nchini Ethiopia, Kenya na Somalia.

Ofisi hiyo imetoa taarifa ikisema katika nchi hizo tatu, watoto wapatao milioni 5.7 wanakumbwa na utapiamlo mkali, wakati mifugo milioni 3 inayotegemewa kimaisha na familia za wafugaji imekufa.

Taarifa hiyo imetolewa kabla naibu katibu mkuu anayeshughulikia mambo ya kibinadamu na mratibu wa mambo ya dharura Bw. Martin Griffiths kufanya ziara ya siku mbili nchini Kenya.

Ofisi hiyo imesema Bw. Griffiths atawasili Nairobi Alhamisi, akiwa na lengo la kuvutia ufuatiliaji wa kimataifa kwa dharura hiyo inayotokana na mabadiliko ya tabianchi, na haja ya kuchukua hatua madhubuti kuokoa maisha ya watu na mifugo.