UM: Tigray yahitaji misaada zaidi ya kibinadamu
2022-05-13 08:53:29| CRI

Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema usambazaji wa misaada ya kibinadamu kwenye eneo la Tigray nchini Ethiopia hautoshi kukidhi mahitaji ya watu.

OCHA imesema kuwa tangu mwanzoni wa Aprili, misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula, vifaa vya matumizi nyumbani na vya elimu imesambazwa katika maeneo yaliyoathiriwa. Katika miezi saba iliyopita, watu karibu milioni 1.5 kaskazini mwa Ethiopia wamepata misaada lakini idadi hiyo ni robo ya jumla ya watu wenye mahitaji.

OCHA imeongeza kuwa kuendelea kusitishwa kwa huduma za kimsingi za benki, umeme na mawasiliano kumezidisha msukosuko wa kibinadamu huko Tigray.

Watu zaidi ya milioni 8 huko kusini mwa Ethiopia pia wanahitaji misaada kutokana na kuathiriwa vibaya na ukame unaoendelea ambao umesababisha watu zaidi ya milioni 15 nchini Ethiopia, Somalia na Kenya kukabiliwa na uhaba wa chakula.