Idadi ya wakenya wanaoathiriwa na ukame yaongezeka hadi milioni 3.5
2022-05-13 08:49:14| CRI

Mamlaka ya usimamizi wa ukame ya taifa ya Kenya imesema wakenya wapatao milioni 3.5 hasa katika maeneo kame au nusu kame, wanakabiliwa na njaa kutokana na maafa hayo.

Mamlaka hiyo imetoa taarifa mpya kuhusu hali ya ukame nchini Kenya, ikisema idadi hiyo imeongezeka kwa watu laki 4 kutoka milioni 3.1 hadi 3.5.

Hali ya ukame inaendelea kuwa mbaya katika kaunti 17 kati ya kaunti 23 zenye ardhi kame au nusu kame, kutokana na upungufu wa mvua mwaka jana na kuchelewa kwa muda mrefu kwa msimu wa mvua wa mwaka huu. Sehemu nane zinazoathiriwa vibaya zaidi na ukame kaskazini mwa Kenya ni pamoja na Marsabit, Mandera, Wajir, Samburu, Isiolo, Baringo, Turkana na Laikipia.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, Kenya imepoteza wanyama milioni 1 wakiwemo ng’ombe, mbuzi, kondoo na ngamia kutokana na ukame katika miezi kadhaa iliyopita.