Balozi wa Mauritius: Mauritius yapenda kuwa daraja kati ya Afrika na China
2022-05-16 14:14:25| CRI

Balozi wa Mauritius nchini China Bw. Marie Roland Alain Wong Yen Cheong hivi karibuni amesema Mauritius ni chaguo bora zaidi kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza barani Afrika, na pia inapenda kuwa daraja kati ya Afrika na China.

Balozi Alain Wong alisema hayo alipohutubia mkutano wa kuhimiza uwekezaji barani Afrika uliofanyika Mei 12 kwa njia ya video. Balozi Wong amepongeza nia ya China ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na kuongeza hali ya kuaminiana kisiasa kati yake na Afrika, na kusema Afrika si kama tu ina hazina kubwa ya maliasili, na bali pia ina mustakbali mzuri kwenye sekta za miundombinu, uchumi wa kibuluu na kilimo.

Balozi Alain Wong amesema Mauritius inajulikana duniani kwa fukwe nyeupe na hoteli za kifahari, lakini katika muongo mmoja uliopita, nchi hiyo pia imetambulika kimataifa kuwa kituo cha fedha cha kimataifa chenye usimamizi bora na kamili. Ameongeza kuwa Mauritius yenye hali maalumu ya kijiografia ina utulivu wa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Mbali hayo, Mauritius ni mwanachama wa makundi ya kiuchumi ya kikanda ikiwemo Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), na imesaini mkataba wa kutotoza ushuru mara mbili (DTA) na mkataba wa kuhimiza na kulinda uwekezaji (IPPA).

Balozi Alain Wong ameeleza kuwa Mauritius imekuwa jukwaa muhimu kwa nchi nyingi ikiwemo China kuwekeza barani Afrika, na asilimia kubwa ya uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni unaoingia Afrika, unafanyika kupitia vyombo vya uwekezaji vya Mauritius. Amesema Mauritius inapenda kutumia fursa mpya ya kuanza kufanya kazi kwa mkataba wa biashara huria kati yake na China, kuzisaidia kampuni za China kupanua wigo wa masoko yao barani Afrika. Ubalozi wa Mauritius nchini China utaanzisha utaratibu wa mawasiliano na ufuatiliaji na wadau wote wenye nia ya kuwekeza barani Afrika kupitia Mauritius.