Waziri wa Biashara na Leba wa Mauritius: Aina 7,500 za bidhaa za Mauritius zinaweza kuingia kwenye soko la China bila ushuru
2022-05-17 10:51:14| CRI

Waziri wa Leba, Maendeleo ya Raslimali Watu na Mafunzo na Waziri wa Biashara na Ulinzi wa Wateja wa Mauritius Bw. Soodesh Satkam Callichurn hivi karibuni amesema, mkataba wa biashara huria kati ya Mauritius na China ulioanza kufanya kazi rasmi mwezi Januari mwaka 2021, umetoa uhakikisho imara wa kimfumo katika kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya pande hizo mbili na kuzinufaisha kwa pamoja. 

Waziri Callichurn alisema hayo kwenye kongamano la kuhimiza uwekezaji barani Afrika, lililofanyika Mei 12 kwa njia ya video. Amesema mkataba wa biashara huria kati ya Mauritius na China, ambao ni wa kwanza kusainiwa kati ya China na nchi ya Afrika, unahusisha nyanja mbalimbali zikiwemo biashara ya bidhaa, biashara ya huduma, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi. Baada ya mkataba huo kuanza kufanya kazi, aina zipatazo 7,500 za bidhaa za Mauritius zinaweza kuingia kwenye soko la China bila ushuru, ambazo ni pamoja na pombe ya miwa, samaki barafu, matunda freshi, juisi, nguo, vitambaa vya kitani, saa na bidhaa za ngozi. 

Bw. Callichurn amesema serikali ya Mauritius inatumai kuijenga nchi hiyo kuwa jukwaa la kikanda kwenye bahari ya Hindi ili kuhimiza biashara na uwekezaji kati ya Afrika na China. Amesema Mauritius inapenda kuendelea kushirikiana na China kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kiutamaduni kati yao, kuhimiza ufufukaji endelevu wa uchumi, kupanua wigo wa biashara na uwekezaji, na kutafuta njia mpya ya maendeleo.