Watu 40 wauawa katika mapigano nchini Burkina Faso
2022-05-17 09:09:12| CRI

Watu 40, wakiwemo mgambo kutoka Ulinzi wa Taifa na raia wa kawaida, wameuawa wikiendi iliyopita katika mashambulizi manne yaliyotokea nchini Burkina Faso.

Kwa mujibu wa jukwaa la habari la “Usalama wa Sahem” linalofuatilia mwenendo wa makundi ya kigaidi, shambulizi la kwanza lililenga msafara uliokuwa unaongozwa na wanajeshi wasaidizi kati ya mji wa Salmossi na Markoye mkoani Oudalan, na kusababisha vifo vya wanajeshi wasaidizi watano na raia mmoja.

Shambulizi la pili lilitokea katika mji wa Guessel, mkoani humo na kuua wanajeshi wasaidizi wanane na raia 12, huku shambulizi la tatu likilenga msafara wa raia uliokuwa ukiongozwa na wanajeshi hao katika mji wa Namouyouri, mkoa wa Kompienga, na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine tisa kujeruhiwa.

Shambulizi la nne lilitokea usiku wa jumamosi na lililenga kikosi cha polisi na vituo vya polisi katika eneo la Faramana mkoani Houet karibu na mpaka wa Mali, ambapo askari polisi wawili walijeruhiwa.