Mkutano wa kilele wa Miji ya Afrika waanza kwa kutoa wito wa kuongeza kasi ya ufufukaji wa miji
2022-05-18 08:47:34| CRI

Mkutano wa tisa wa kilele wa Miji ya Afrika umeanza jana mjini Kisumu nchini Kenya, na kutoa wito wa kuboresha ufufukaji wa miji ili kukabiliana na umasikini na magonjwa huku ikiimarisha unyumbukaji wa jamii husika.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo, rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesisitiza kuwa sera bora, ufadhili wa uvumbuzi na uhusiano ni mambo muhimu katika kutimiza miji endelevu ya kisasa barani Afrika. Amesema kukua kwa kasi kwa miji katika bara hilo kunapaswa kutumika kama kichocheo kwa watungasera, wawekezaji na wafadhili wa pande nyingi kutoa mipango ya kukabiliana na uchafuzi wa hewa, ukosefu wa ajira na uhaba wa mahitaji muhimu kama maji na makazi.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amesema, utekelezaji wa ajenda ya miji ya kisasa katika bara la Afrika umeshika kasi, na unaendana na haja ya mabadiliko ya kiuchumi na kijamii pamoja na mabadiliko ya tabianchi.