Benki ya Dunia kuendelea kufadhili miradi inayounga mkono watu masikini nchini Sudan
2022-05-18 08:46:34| CRI

Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imetangaza kuwa, Benki ya Dunia imearifu mamlaka za nchi hiyo kuwa itaanza tena kufadhili miradi inayounga mkono watu masikini nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo imesema, Benki ya Dunia inaendelea na hatua za kuanza tena ufadhili wa miradi inayolenga moja kwa moja kuwasaidia watu masikini nchini Sudan, ikiwemo program ya Thamrat na chanjo dhidi ya virusi vya Corona, kupitia utekelezaji na usimamizi unaofanywa na upande wa tatu kama vile Mpango wa Chakula Duniani.

Kwa mujibu wa utafiti wa Benki ya Dunia, asilimia 30 ya Wasudan hawana uwezo wa kununua mahitaji yao ya lazima baada ya kutekeleza mageuzi ya kiuchumi.

Sudan imeingia kwenye mgogoro wa kiuchumi tangu kujitenga na Sudan Kusini mwaka 2011, na kuigharimu nchi hiyo asilimia 75 ya kipato kinachotokana na mafuta.