Waziri wa Huduma za Fedha wa Mauritius: Mauritius itaendeleza ushirikiano wenye mtazamo wa mbali na China
2022-05-19 09:51:02| CRI

Waziri wa Huduma za Fedha na Utawala Bora wa Mauritius Bw. Mahen Kumar Seeruttun, amesema serikali ya Mauritius itaendelea kuweka mkazo katika kuhimiza biashara na uwekezaji kati yake na China, na kuendeleza ushirikiano wenye mtazamo wa mbali na China.

Waziri Seeruttun alisema hayo kwenye kongamano la kuhimiza uwekezaji barani Afrika, lililofanyika Mei 12 kwa njia ya video. Amesema uhusiano kati ya Mauritius na China una historia ndefu, na Mauritius ina moja ya mitaa mikongwe zaidi ya jamii ya watu wenye asili ya China (China town) barani Afrika. Wahamiaji wengi kutoka China wameweka msingi imara wa kukuza uhusiano wa nchi hizo mbili, haswa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara. Amesema serikali ya Mauritius na watu wake wote wameona mustakbali mkubwa wa kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi na China. Kwa mfano, Mkataba wa Biashara Huria kati ya Mauritius na China una vipengele kuhusu huduma za kifedha, ikiwemo kuendeleza huduma na miundombinu ya kuwezesha malipo ya sarafu ya China RMB nchini Mauritius.

Bw. Seeruttun amesema serikali ya Mauritius siku zote imekuwa inajitahidi kutoa vibali vya biashara, msamaha wa kodi na nafuu nyingine kwa kampuni za kimataifa zenye biashara nchini Mauritius, na kampuni nyingi kubwa za China zimeweka matawi yao nchini Mauritius, ikiwa ni pamoja na kampuni ya Huawei iliyoweka ofisi nchini Mauritius mwaka 2004 na kutoa huduma kwa nchi zaidi ya 50 za Afrika kupitia kituo chake nchini humo, na Benki ya China iliyoanzisha tawi lake nchini mwaka 2016 na kuwa jukwaa muhimu la kuwekeza barani Afrika. Waziri Seeruttun amezikaribisha kampuni nyingi zaidi za China kuwekeza na kuanzisha biashara nchini Mauritius, na kutumia jukwaa la Mauritius kupanua wigo wa biashara zao katika bara zima la Afrika.