Zimbabwe yafanya mkutano wa kilele wa tembo kujadili usimamizi wa tembo
2022-05-24 09:15:14| CRI

Mkutano wa kilele wa tembo umefunguliwa jana Jumatatu katika mbuga ya wanyamapori ya taifa ya Hwange nchini Zimbabwe, ambapo nchi zinazoshiriki zimetaka kufikia makubaliano kuhusu usimamizi wa tembo na hifadhi ya wanyamapori.

Mkutano huo utakaoendelea hadi Mei 26 utakuwa jukwaa la kujadili mzigo wa ongezeko la kupita kiasi la tembo na athari zinazotokana na marufuku dhidi ya biashara ya kimataifa kuhusu pembe za ndovu.

Mbali na hayo nchi zinazoshiriki zinataka kufikia makubaliano ya pamoja kabla ya mkutano wa 19 wa pande mbalimbali za Makubaliano ya Biashara ya Kimataifa kuhusu Spishi zilizo Hatarini CITES.

Nchi za magharibi na wanaharakati wa haki za wanyama siku zote wanapinga biashara za pembe za ndovu, huku wakiona kuwa ongezeko la uwindaji haramu linatishia maisha ya tembo wa Afrika. Lakini walinzi wa wanyamapori wa Zimbabwe wanaendelea kutetea kuwa mauzo ya pembe za ndovu zenye thamani ya dola milioni 600 za kimarekani zinazohifadhiwa nchini humo yatasaidia kufadhili juhudi za kuhifadhi wanyamapori.