Rais Mwinyi azindua tamasha la Sanaa na Utamaduni visiwani Zanzibar
2022-05-24 09:23:47| CRI

Rais wa Zanzibar, Tanzania Hussein Ali Mwinyi jana Jumatatu alizindua tamasha la Sanaa na Utamaduni la Afrika lijulikanalo kwa jina la Festac Africa 2022, na kuzitaka serikali za nchi Afrika kuhimiza ustawi wa Sanaa na Utamaduni ndani ya bara hilo.

Rais Mwinyi alisema tamasha hilo limewashirikisha  zaidi ya wasanii 10,000 kutoka Afrika nzima, linapaswa kutumika kama chombo cha kuhimiza ushirikiano na biashara kati ya nchi za Afrika. Amebainisha kuwa tamasha hilo  linalounganisha tamaduni za Afrika limekuja kwa wakati muafaka na ni muhimu kwa juhudi zinazoendelea kufanywa  na mamlaka za Zanzibar ili kurudisha shughuli za utalii baada ya kuathiriwa na janga la UVIKO-19. Ametumai  washiriki kujifunza historia, Sanaa na utamaduni wa Zanzibar na kuwa mabalozi  katika nchi zao na pia kuitangaza Zanzibar kama kituo cha utalii.

Abdulrazak Gurnah, mshindi wa tuzo ya Nobel ya Fasihi mwaka 2021, ni miongoni mwa wasanii maarufu walioshiriki kwenye  tamasha hilo, ambalo litaonesha Sanaa, utamaduni, urithi, muziki, utalii, sekta ya huduma na usafiri .