Mlinda amani wa Zimbabwe kupokea Tuzo ya Mtetezi wa Jinsia wa Kijeshi ya UM kwa mwaka 2021
2022-05-25 10:34:32| CRI

Idara ya Operesheni za Amani imesema mlinda amani wa Zimbabwe atapokea Tuzo ya Umoja wa Mataifa ya Mtetezi wa Jinsia wa Kijeshi ya mwaka 2021.

Mwangalizi wa Kijeshi Meja Winnet Zharare mwenye umri wa miaka 39, alifanyakazi Bentiu, Sudan Kusini hadi mwaka 2022 na atapokea tuzo hiyo kutoka kwa Katibu Mkuu wa UM Antonio Guterres kwenye sherehe ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa kesho Alhamis.

Kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari Guterres amesema kupitia kazi yake, ameonesha jukumu kubwa kwamba wanawake wanabeba wajibu wa kujenga uaminifu, kutetea mabadiliko na kuleta amani akiongeza kuwa mfano wake unaonesha jinsi watu wote watakavyonufaika kukiwa na wanawake wengi zaidi kwenye meza za kutoa maamuzi na kutetea usawa wa kijinsia katika operesheni za amani.

Zharare alipelekwa kwenye Tume ya Kulinda Amani nchini Sudan Kusini mwezi Novemba 2020. Kupitia kipindi chake cha utendaji kazi cha miezi 17, alitetea usawa wa kijinsia na ushiriki wa wanawake kwa wanajeshi wenzake na kwenye jamii za wenyeji.