Tunisia yaandaa kongamano la uchumi kuhimiza biashara na uwekezaji barani Afrika
2022-05-26 10:50:19| CRI

Kongamano la 5 la uwekezaji wa kifedha na biashara barani Afrika (FITA 2022) limefunguliwa jana nchini Tunisia, ili kuhimiza biashara na uwekezaji barani Afrika.

Akifungua kongamano hilo la siku mbili, Waziri Mkuu wa Tunisia Najla Bouden Romdhane alisema kuwa watu wapatao 3500 kutoka nchi 45 wakiwemo mawaziri wa nchi za Afrika na viongozi wa mashirika na taasisi za kimataifa wanashiriki kwenye kongamano hilo.

Amesisitiza kuwa janga la COVID-19 na mgogoro kati ya Ukraine na Russia, pamoja na ongezeko la bei ya maliasili, vyakula na mafuta zimedhoofisha uchumi wa nchi za Afrika.

Pia ametoa mwito wa kutolewa nadharia mpya na zenye uvumbuzi ili kuinua ushindani wa Afrika na kuimarisha maendeleo yake ya kijamii na kiuchumi, ongezeko la uchumi, uwekezaji na biashara.