Tanzania yatoa tahadhari kuhusu ugonjwa wa monkeypox
2022-05-27 09:19:45| CRI

Mamlaka za Afya Tanzania Alhamis zilitoa tahadhari juu ya ripoti ya mlipuko wa ugonjwa wa monkeypox katika baadhi ya nchi za Ulaya.

Kwenye taarifa yake Naibu Waziri wa Afya wa Tanzania Bw. Godwin Mollel amesema kwamba umma unahitaji kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo na magonjwa mengine ya kuambukiza.

Amewatoa wasiwasi watu kwa kusema kwamba hadi sasa hakuna wagonjwa wa monkeypox walioripotiwa nchini Tanzania, lakini amewatahadharisha wananchi kuepuka kugusa au kula wanyama wenye ugonjwa, pamoja na kuepuka kugusa kitu chochote ambacho kimetumiwa na wanyama wenye ugonjwa.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa kesi nyingi za maambukizi ya ugonjwa huo zitaripotiwa, huku nchi 20 duniani zikiwa tayari zimesharipoti. Dalili za awali za ugonjwa wa monkeypox ni homa, maumivu ya kichwa, uvimbe, maumivu ya mgongo, maumivu ya misuli na uchovu. Na watu walio na ugonjwa mbaya zaidi wanaweza kupata vipele na vidonda kwenye uso na mikono, kisha kuenea kwenye sehemu nyingine za mwili.