Vikosi vya kulinda amani vya China vyachangia amani na usalama barani Afrika
2022-05-30 08:31:17| CRI

Huu ni mwaka wa 30 tangu China ilipoanza kupeleka vikosi vya kulinda amani kwa nchi za nje. Ikiwa moja ya nchi kubwa zaidi duniani, katika miaka 30 iliyopita, China imetekeleza kikamilifu wajibu wake wa kimataifa, na kutoa mchango muhimu katika kudumisha amani na utulivu duniani, hasa barani Afrika, kwa vitendo halisi.

Hivi sasa, China ina zaidi ya wanajeshi 2,000 wa kulinda amani barani Afrika, ambao ni zaidi ya asilimia 75 ya walinda amani wote wa Umoja wa Mataifa barani Afrika, na zaidi ya asilimia 80 ya walinda amani wa China walio nje ya nchi. Askari hao wa kulinda amani wa China wanalinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Liberia, Sudan, Sudan Kusini, Mali, Libya na Jamhuri ya Afrika ya Kati na nchi nyingine za Afrika zinazokumbwa na vita na migogoro.

Kwa sasa, China ni nchi iliyotuma walinzi wengi zaidi wa amani kati ya nchi wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na pia ni nchi ya pili katika utoaji wa fedha kwa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa. China siku zote imekuwa mjenzi wa amani ya dunia, mchangiaji wa maendeleo ya kimataifa, na mtetezi wa utaratibu wa kimataifa. Katika siku zijazo, wanajeshi wengi zaidi wa China watajitolea kuchangia katika kudumisha amani na utulivu duniani, haswa barani Afrika.