AU yatoa wito kwa Rwanda na DRC kujizuia na kufanya mazungumzo ili kutatua mgogoro kwa amani
2022-05-30 10:00:36| CRI


 

Mwenyekiti wa zamu wa AU ambaye pia ni rais wa Senegal Macky Sall amesema ana wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mvutano kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kutoa wito kwa nchi hizo mbili kujizuia na kufanya mazungumzo ili kutatua mgogoro huo kwa amani.

Habari zinasema hapo awali jeshi la Ulinzi la Rwanda lilisema wanajeshi wake wawili walitekwa nyara na kushikiliwa mashariki mwa DRC na kikosi cha serikali (FARDC) kilichokuwa kwenye doria. Tarehe 23 mwezi Mei kikosi hicho kilifanya mashambulizi ya makombora kuvuka mpaka na kuwajeruhi raia.

DRC inashutumu serikali ya Rwanda kwa kuliunga mkono kundi la waasi la M23, ambalo limepambana na wanajeshi wa serikali ya DRC kwa takriban wiki moja, na kusababisha watu wasiopungua elfu 70 kupoteza makazi yao.

Hadi sasa DRC imechukua hatua dhidi ya Rwanda, ikiwemo kukutana na balozi na kusimamisha safari za ndege na nchi hiyo. Shirika la ndege la Rwanda limetangaza kufuta mara moja safari zote za Kinshasa, Lubumbashi na Goma.