Kenya yapanga kuuza nje maua kupitia reli ya SGR kufikia mwisho wa mwaka 2022
2022-05-31 08:58:53| CRI

Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Maua la Kenya (KFC) Bw. Clement Tulezi amesema kuwa Kenya inapanga kuanza kuuza nje maua yake yaliyohifadhiwa kwenye makontena ya baridi kupitia reli ya SGR hadi bandari ya Mombasa na kusafirishwa kwenda Ulaya ifikapo mwishoni mwa mwaka 2022.

Akiongea wakati wa hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya Biashara ya Maua ya Kimataifa (IFEX), Tulezi amebainisha kuwa usafirishaji wa bidhaa freshi kwa njia ya reli pia ni bora kwa mazingira kwa sababu ya utoaji mdogo wa kaboni ukilinganishwa na usafiri wa barabarani au wa anga. Katika mwaka 2021, maua yalikuwa chanzo kikubwa cha mapato ya fedha za kigeni nchini Kenya baada ya chai, na kuipatia nchi hiyo dola za kimarekani milioni 934.

Maua mengi ya Kenya yanasafirishwa kwa ndege ambayo ni njia haraka ya usafiri. Lakini janga la COVID-19 liliibua vikwazo vya utumiaji ndege kwani safari nyingi za ndege zilisitishwa na kusababisha kupungua kwa kasi usafirishaji wa mizigo kwa ndege.

Ameongeza kuwa gharama ya usafirishaji wa maua freshi kupitia SGR ni nafuu na haraka ikilinganishwa na usafirishaji wa malori ya masafa marefu.