Benki kuu ya Kenya imekadiria kuwa uchumi utaongezeka kwa asilimia 5.7 mwaka 2022, ambayo ni chini ikilinganishwa na asilimia 7.5 ya mwaka 2021.
Akiongea na vyombo vya habari baada ya mkutano wa Kamati ya Sera ya Fedha (MPC), Gavana wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) Bw. Patrick Njoroge amesema viashiria vikuu vya kiuchumi vimeonyesha katika robo ya kwanza ya mwaka 2022 uchumi ulifanya vizuri.
Njoroge ameongeza kuwa ingawa dunia inakabiliwa na uwezekano wa kupungua kwa ukuaji wa uchumi, ukuaji wa uchumi wa Kenya unatarajiwa kubaki imara mwaka 2022.
Ameeleza kuwa sekta nyingine zinatarajiwa kukua kwa kasi zaidi ikilinganishwa na sekta ya kilimo ambayo inategemea sana mvua, na sekta zinazotarajiwa kufanya vizuri zaidi ni za huduma za malazi na chakula ambazo zitafufuka baada ya kulegeza vizuizi vilivyowekwa wakati wa janga la COVID-19.