Watu milioni 7.7 wahitaji msaada wa kibinadamu nchini Somalia
2022-06-01 08:53:59| CRI

Idadi ya jumla ya watu wanaohitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi nchini Somalia imeongezeka hadi milioni 7.7 kutoka milioni 5.9 ya mwaka 2021.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilisema ukame unaoongezeka ambao umekumba maeneo kadhaa ya Somalia kutokana na uhaba wa mvua umeharibu maisha ya watu wengi nchini Somalia.

OCHA ilisema katika ripoti yake mpya kuhusu ugawaji wa fedha za msaada wa kibinadamu kuwa idadi ya watu walioathirika inaongezeka kwa kasi, na familia zilizokimbia makazi zinakaribia viwango vya kutishia maisha.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, ukame mkali unazidisha athari na mahitaji ya kibinadamu yaliyosababishwa na migogoro na ukosefu wa usalama, pamoja na majanga ya hali ya hewa na milipuko ya magonjwa iliyodumu kwa miongo kadhaa.

OCHA ilisema dola za Kimarekani milioni 25 zitatolewa kama msaada wa haraka kwa jamii zilizoathiriwa vibaya na ukame katika maeneo muhimu, haswa yale ambayo hayajashughulikiwa na ni vigumu kufikiwa.