Rais wa Zanzibar aamuru kufanywa msako wa bandari haramu
2022-06-01 08:52:46| CRI

Rais wa Zanzibar ambaye pia ni  Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi jana Jumanne aliamuru mamlaka za utekelezaji wa sheria zikiwemo polisi na jeshi kuanza msako juu ya bandari haramu, kabla hali haijawa mbaya zaidi.

Amri hiyo ameitoa kwenye hotuba yake ya kila mwezi kwa wanahabari huko Ikulu ya Vuga, ambapo amebainisha kuwa kuna idadi kubwa ya bandari haramu visiwani Zanzibar zinazotumika kusafirisha bidhaa za magendo nje ya visiwani au kuingiza bidhaa bila ya kulipa ushuru. Amesema wafanyabiashara wanaotumia bandari hizo wanasababisha hasara kubwa kwenye mapato ya serikali.

Ingawa Dkt Mwinyi hakutaja idadi ya bandari haramu visiwani Zanzibar, lakini uchunguzi uliofanywa na Mamlaka ya Bandari Zanzibar (TPA) mwaka 2018 umebainisha bandari haramu 134 kwenye fukwe za ziwa na bahari ya Hindi. Uchunguzi  huo unaonesha kuwa bandari hizo zimekuwa zikitumika kusafirisha bidhaa za magendo, zikiwemo sukari, mafuta ya kupikia, saruji, mbao, madini na nyingine nyingi ambazo zinahatarisha kuua viwanda vya ndani.