Zaidi ya hekta 51,000 za ardhi nchini Ethiopia zashambuliwa na wadudu
2022-06-03 09:19:01| CRI

Mkurugenzi wa ulinzi wa mimea katika Wizara ya Kilimo ya Ethiopia, Belayneh Negussie amesema zaidi ya hekta 51,000 za ardhi nchini humo zimeshambuliwa na wadudu katika siku za karibuni.

Akitaja maeneo hayo ambayo ni ya mikoa ya Gambella, Benishangul-Gumuz na Amhara, Bw. Negussie amesema kati ya hekta 51,209 za mashamba yaliyoshambuliwa na wadudu, hekta 23,219 zimepuliziwa dawa za kuzuia wadudu kwa njia za jadi na kisasa. Pia amebainisha kuwa safari hii Ethiopia imeshambuliwa vibaya zaidi na wadudu katika miaka miwili iliyopita, ambapo juhudi zinaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha mazao hayapotei kwenye maeneo yaliyoshambuliwa na wadudu.

Wizara ya Kilimo ya Ethiopia pia inafanya kazi za maandalizi zikiwemo kupulizia dawa za kemikali katika sehemu nyingine za nchi hiyo, ambazo zinaonekana ni rahisi sana kushambuliwa na wadudu. Aidha wizara inawahamasisha wakulima kudhibiti wadudu kwa njia za jadi ili kupunguza athari za uvamizi wa wadudu mashambani.