China yatoa wito wa kutatuliwa mgogoro wa mashariki mwa DRC kwa mazungumzo
2022-06-03 09:16:33| CRI

China imetoa wito wa kutatuliwa kwa mazungumzo ya amani mgogoro unaozidi kuongezeka katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC ili kurudisha utulivu wa kanda hiyo mapema.

Hivi karibuni, mashambulizi yaliyofanywa na wapiganaji wa kundi la waasi dhidi ya raia na walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa yamesababisha vifo vya watu na kuzorota usalama katika eneo la mashariki mwa DRC, na kwamba serikali za DRC na Rwanda zinalaumiana na kuzidisha mvutano kati ya nchi hizo mbili.

Juu ya hili, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Bw. Zhao Lijian jana alisema China ina wasiwasi na hali ya usalama inayozidi kuwa mbaya katika eneo hilo, na kupinga mashambulizi yoyote dhidi ya raia na walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa. Amesema China inapenda kufanya juhudi za kuleta amani na maendeleo katika eneo la mashariki mwa DRC na kushirikiana na jamii ya kimataifa kutoa mchango wa kiujenzi kuhusu masuala husika.