ECOWAS yakataa kipindi cha mpito cha miezi 36 kilichopendekezwa na viongozi wa kijeshi wa Guinea
2022-06-06 09:04:34| cri

Rais wa Kamati ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) Bw. Jean-Claude Kassi Brou amesema, Jumuiya hiyo imekataa pendekezo la viongozi wa kijeshi wa Guinea la kipindi cha mpito cha miezi 36, na kutaka mashauriano yaendelee kutafuta suluhu ya ratiba hiyo.

Bw. Brou ametoa wito kwa Guinea kushughulikia mgogoro wa kijamii na kisiasa kati ya serikali, mashirika ya kiraia na makundi mengine husika.

Septemba 5 mwaka jana, Luteni Kanali Mamady Doumbouya alitangaza kuwa jeshi la nchi hiyo linamshikilia rais Alpha Conde na kuvunja serikali yake pamoja na taasisi nyingine za kitaifa.

ECOWAS ilijibu tukio hilo kwa kutangaza kusitisha uanachama wa Guinea katika Jumuiya hiyo na pia kuweka vikwazo kwa viongozi wa mapinduzi hayo ya kijeshi.