Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaonya juu ya janga la njaa linaloinyemelea Somalia
2022-06-07 09:05:38| CRI

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) yameonya juu ya baa la njaa linaloinyemelea Somalia kufuatia uhaba wa mvua kwa msimu wa nne mfululizo, na kutoa wito wa uungaji mkono zaidi ili kukwepa janga hilo.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa jana mjini Mogadishu na Mkurugenzi wa WFP nchini Somalia El-Khidir Daloum, mashirika hayo yamesema hatua zinatakiwa kuchukuliwa mara moja ili kukwepa janga la kibinadamu, na kuongeza kuwa maisha ya makundi yaliyo hatarini tayari yanakabiliwa na tishio la utapiamlo na njaa.

Mashirika hayo yamesema, ukosefu wa mvua kwa misimu minne mfululizo, kuongezeka kwa bei za vyakula, na mwitikio mdogo wa kukabiliana na mgogoro wa kibinadamu vimesababisha ongezeko la asilimia 160 la watu wanaokabiliwa na ukosefu wa chakula, njaa, na magonjwa nchini Somalia.